By News Desk
Mwanabiashara maarufu na mwanasosholaiti wa Afrika Mashariki, Zari Hassan, maarufu kama Zari The Boss Lady, amethibitisha rasmi kuwa ameachana na mume wake wa tatu, Shakib Cham, baada ya miaka mitano ya kuwa pamoja.
Tangazo hilo linakuja kufuatia miezi kadhaa ya uvumi kuhusu changamoto zilizokuwa zikikumba ndoa yao. Hapo awali, wawili hao walikuwa wakikanusha madai ya kutokuelewana na kusisitiza kuwa walikuwa bado imara kama familia.
Katika taarifa yake, Zari alisema kuwa uamuzi wa kuachana ulifikiwa baada ya kutafakari kwa kina kuhusu mustakabali wa uhusiano wao.
“Baada ya miaka mitano ya kutafakari kwa kina na kuangalia safari yetu, tumegundua kuwa ni bora kila mmoja aendelee na maisha yake kwa sababu kuna mambo ambayo hatukuweza kuyakubaliana. Haikuwa uamuzi rahisi, lakini tunaamini ndiyo njia bora kwetu sote,” alisema Zari.
Zari, ambaye ni mama wa watoto watano na mmoja wa wanawake wenye ushawishi mkubwa katika mitandao ya kijamii Afrika Mashariki, amekuwa akivutia umakini wa umma kutokana na maisha yake binafsi na safari yake ya biashara. Uhusiano wake na Shakib Cham ulionekana kuwa mfano wa mapenzi yaliyovuka tofauti ya umri, huku Shakib akiwa mdogo kwa miaka 12 kuliko Zari.
Habari za kutengana kwao zimezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa burudani, wengi wakionyesha mshangao huku wengine wakitoa salamu za heri kwa wawili hao wanapoanza sura mpya za maisha yao.
Licha ya kuvunjika kwa ndoa hiyo, Zari amesisitiza kuwa uamuzi huo umefanywa kwa heshima na maelewano, akieleza kuwa wote wawili wanaendelea kuthaminiana na kutakiana mema katika maisha yao yajayo.
